TADB KUWANUFAISHA WANAWAKE WENYE MIRADI YA KILIMO NDANI YA MINYORORO YA THAMANI

Benki ya Maendeleo Ya Kilimo Tanzania (TADB) kupitia ofisi zake za kanda ya nyanda za juu kusini imefanya ziara ya kutembelea miradi ya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo mkoani Songwe na Njombe.

TADB inaamini kilimo kitabenkika zaidi iwapo uwekezaji utafanyika katika kila hatua ya mnyororo wa thamani ya mazao, hasa kuwezesha viwanda vidogo, na vya kati ili kuongeza mahitaji ya bidhaa na mali ghafi za kilimo.

Uwekezaji katika viwanda vidogo na vya kati huchochea uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia kilimo na kuwainua wakulima na wananchi wa chini kabisa wakiwemo wanawake. Katika ziara hiyo, TADB ilitembelea mradi wa kulima, kuchakata na kusaga kahawa unaoendeshwa na kampuni ya GDM iliyopo mkoani Songwe. Kampuni ya GDM, ina zaidi ya waajiriwa 250 na kati ya hao asilimia 80% ni wanawake.

TADB pia ilitembelea mradi wa Mama Seki Group ambapo pia asilimia kubwa ya shughuli za mradi zinafanywa na wanawake. Mama Seki Group ni moja ya viwanda vidogo vinavyomilikiwa na wanawake , vilivyowezeshwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania katika mkakati wake wa kuwainua wanawake kiuchumi.

Benki ya Maendeleo Ya Kilimo Tanzania (TADB) ina mikakati ya makusudi ya kuwainua wanawake na vijana wengi zaidi nchini wenye utashi wa kujishughulisha na kazi zinazohusiana na kilimo, kama uzalishaji mbegu, utunzaji mashamba, kumiliki maghala ya kuhifadhia chakula, kuchakata mali ghafi na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kama ilivyo kwa Mama Seki Group na GDM.