Waziri Mkuu azindua kongani

WAZIRI MKUU AZINDUA KONGANI YA TADB KANDA WA ZIWAWaziri Mkuu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo nchini (TADB) ili kujenga Tanzania ya viwanda. Ametoa wito huo wakati akizindua Ofisi ya TADB Kongani ya Kanda ya Ziwa inayohudumia mikoa ya Kagera, Shinyanga, Geita, Mara, Simiyu na jiji la Mwanza ambapo itakuwa makao makuu ya kongani hiyo.

Waziri Mkuu amesema kuwa uchumi wa viwanda unategemea sana sekta ya kilimo kwa ajili ya malighafi hivyo, ni wakati muafaka kwa Watanzania kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji mazao, mifugo na uvuvi ni muhimu sana katika kuhakikisha usalama wa chakula. “Kutokana na umuhimu huo, nawasihi kuchangamkia nafasi hii ya uwepo wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ambayo ni benki mama kwa mipango inayolenga kutatua changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini,” alisema.

Aidha, ameongeza kuwa uwezeshaji katika sekta ya kilimo ambayo inachangia zaidi ya asilimia 60 ya ajira nchini, na asilimia isiyopungua 80 ya mauzo ya nje yaani ‘exports’ na pia inachangia zaidi ya asilimia 60 ya mali ghafi zinazotumiwa na viwanda kutaleta tija katika kupambana na umaskini, ukosefu wa ajira na katika kuleta maendeleo ya nchi. “Halikadhalika, naendelea kuwasihi TADB kushirikiana na wadau wengine katika kutatua changamoto za kilimo nchini ili tuweze kufikia ndoto yetu ya kuwa nchi ya uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025,” aliongeza.

Kwa upande wake, Naibu wa Waziri wa Kilimo, Mhe. Innocent Bashungwa alisema kuwa TADB imekuwa ikitekeleza dhana ya uchumi wa viwanda kwa kushiriki katika utekelezaji wa Mpango wa Kilimo wa Awamu ya Pili (ASDP II). Kwa mujibu wa Naibu Waziri hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu, Benki ya Maendeleo ya Kilimo imeshatoa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kutekeleza malengo mbalimbali kama ilivyoainishwa na ASDP II.

“Tunaishukuru TADB kwa kuwawezesha wakulima nchini katika ununuzi wa matrekta na zana za kilimo ikiwemo matrekta na zana nyinginezo pamona na mikopo kwa ajili ya mikopo ya viwanda vya kusindika mazao ya chakula,” alisema.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Rosebud Kurwijila alisema Benki ya Maendeleo ya Kilimo iliamua kuanzisha dhana ya kongani mara baada ya kukabiliana na changamoto kubwa ya jinsi ya kufikia nchi nzima, ambapo wataalam nchini waliishauri kutumia mfumo wa kongani (yaani Clustering and Value chain financing approach). Aliongeza kuwa mfumo huu hufikisha huduma karibu na wateja kwa kuzingatia mfanano (similarities) wa mazao ya vipaumbee hali ya hewa (climatic conditions) na tamaduni za maeneo husika.

“Tunaamini pia kuwa mfumo huu wa kongani utatuwezesha kutandaa vizuri nchini huku tukiwezesha kuanzisha “agricultural parks” za kimkakati katika kila kongani zitakazokidhi hamu ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwa na viwanda vikubwa vinavyotokana na mazao ya kilimo katika kila kongani,” alisema.

Akitoa taarifa ya mafanikio ya Benki hiyo tangu ilipoanzishwa, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine alisema hadi kufikia tarehe 28 Februari 2019, Benki hiyo imefanikiwa kukuza mtaji wake na kufikia kiasi cha Shilingi 68 Billioni ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia kumi kutoka mtaji wa Shilingi 60.0 Bilioni uliolipwa na Mwenye Hisa yaani Serikali ya Tanzania mwaka 2015.

“Ukuaji wa mtaji wa Benki umechangiwa kwa kiasi kikubwa na malimbikizo ya faida iliyotengenezwa katika kila mwaka wa fedha tangu Benki ilipoanza shughuli zake mwaka 2015,” alisema. Aliongeza kuwa upande wa utoaji wa mikopo ya kimkakati, hadi kufikia tarehe 28 Februari 2019, TADB ilifanikiwa kupanua huduma zake na kutoa mikopo ya Shilingi Bilioni 100.7 ikiwa ni ongezeko la mikopo ya Shilingi Bilioni 67.5 katika kipindi cha miezi minane kutoka mikopo ya Shilingi 33.2 Bilioni iliyotolewa hadi kufikia 31 Juni 2018.

“Aidha, hadi kufikia 28 Februari 2019, TADB ilikuwa imeshatoa mikopo kwa ajili ya kuendeleza miradi 84 ya mazao mbalimbali nchini na kunufaisha jumla ya wakulima 837,578,” “Katika mikopo yote iliyotolewa, kiasi cha shillingi bilioni 31.4 kimeweza kurejeshwa kutoka kwa wateja na mpaka mwisho wa mwezi Februari 2019, kiasi cha mikopo chechefu kilikuwa asilimia 2.5 ambayo ni chini sana ikilinganishwa na wastani wa zaidi ya asilimia 10 kwa mabenki mengine nchini,” aliongeza.

Justine aliongeza katika Kongani ya Kanda ya Ziwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo katika msimu wa pamba wa 2018 ilitoa mkopo wa gharama nafuu ili kufanikisha ununuzi na usambazaji wa viatilifu vya zao la pamba kwa wakulima katika mikoa 17 na wilaya 49 nchini ikiwemo mikoa yote ya Kongani ya Kanda ya Ziwa. “Mkopo huu ulichangia kwa kiasi kikubwa ongezeko kubwa la uzalishaji ambapo kwa msimu wa pamba wa 2018, mavuno ya pamba yalifika tani 221,600 ikiwa ni ongezeko la asilimia 67 ilikilinganishwa na tani 133,000 zilizozalishwa msimu wa 2017,” alisema.