WAKULIMA WADOGO WADOGO KUANZA KUNUFAIKA KUPITIA MKAKATI WA BENKI YA MAENDELEO YA KILIMOMkurugenzi wa mikopo na biashara wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, ndugu Augustino Matutu Chacha, alifanya ziara mkoani Dodoma na Singida kwa kuitembelea miradi mbalimbali inayoongeza thamani katika mazao ya kilimo yanayozalishwa na wakulima wadogo wadogo na AMCOs. Lengo kubwa la ziara hii ni kujifunza namna miradi hii inavyoendeshwa, na kuangalia namna ya kufungua fursa za masoko na uzalishaji kwa wakulima wadogo pamoja na AMCOS.

Moja ya miradi na viwanda alivyotembelea ni pamoja na PYXUS Agriculture Tanzania, kiwanda cha uzalishaji Mafuta ya alizeti ya mkoani Dodoma. Moja ya majadiliano ni kuangalia namna ya kufanya kazi pamoja na kufungua masoko ya wakulima wadogo wa alizeti wa mkoa wa Singida ambao tayari wamewezeshwa na benki ya TADB kwa huduma za mikopo na fedha.

Hii ni moja ya ubunifu wa huduma unaofanywa na Benki ya maendeleo ya Kilimo Tanzania katika kuongeza wigo wa fursa kwa wakulima wadogo kwa kuwaunganisha na viwanda vya jirani ya mikoa na vijiji vyao. Jitihada hizi zinafanywa ili kuwawezesha wakulima wadogo kuongeza uzalishaji wa mazao, kupata masoko ya uhakika pamoja na kujipatia ajira endelevu.