Trekta Md 2

TADB YAWATANGAZIA NEEMA WAKULIMA WANAOHITAJI MATREKTA

KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Kilimo(TADB), Bw.
Japhet Justine ameshauri watanzania kujikita  zaidi kwenye kilimo
kwani kinalipa huku akisema benki yake ipo tayari kutoa fedha asilimia
80 kwa wanaohitaji kukopa matrekta na asilimia 20 iliyobaki itatolewa
na mnunuzi.

Akizungumza  Kibaha mkoani Pwani mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango,Bw. Dotto James , Bw. Justine amesema benki yake
imejipanga kuinua sekta sekta ya kilimo na mkulima mwenyewe hivyo
matrekta yatawasidia kurahisha kazi badala ya kutumia jembe la mkono.

“Kikubwa ambacho  sisi kama benki tunataka kuona  mkulima anafanikiwa
kupitia mazao yake na kubadilisha maisha na kujenga uchumi imara.
Mkulima ana nafasi kubwa sana katika ujenzi wa uchumi wa kati na wa
viwanda ifikapo mwaka 2025,” alisisitiza.

Akifafanua zaidi, Bw. Justine alisema TADB  imeshatoa mkopo wa
Sh.bilioni 41.1 tangu kuanzishwa kwa benki hiyo na tayari ipo kwenye
mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma.

“Tunatarajia kufungua tawi lingine mkoani Mbeya hivi karibuni na lengo
letu ni kuwafikia wananchi popote walimo nchi nzima,” bosi wa benki
alisema na kuongeza kuwa sekta ya kilimo ni muhimu sana katika sekta
yeyote ya viwanda duniani.

Bw. Justine alisema TADB imeingia makubaliano na Shirika la Maendeleo
la Taifa(NDC) kwa lengo la kusaidia wale wanaonunua matrekta ambapo
benki ya kilimo itaingiza asilimia 80 ya mkopo na mnunuzi atatoa
asilimia 20.

Alisema kuwa  wakulima wamefanya vizuri kwenye zao la pamba huku
akielezea lengo la benki  kuchoche na kuhamasisha kilimo cha kisasa
zaidi  ili kumuondoa mkulima kwenye jembe la mkono.

“Pale tutakapofanikiwa kumtoa mkulima kwenye jembe la mkono na kumpa
mashine ambazo zitamsaidia kuongeza tija, ufanisi na kumpa faida zaidi
hicho ndicho benki inapenda kuona mkulima anafanikiwa,” alisisitiza.

Alisema  benki yake  itaanza na matrekta 500 ambayo  watapewa wakulima
waliofanya vema kwenye kilimo cha pamba ili kuchochea uzalishaji zaidi
wa zao hilo na mazaa mengine sehemu mbalimbali nchini.

“ Tuna mpango  kwenda kuziambia benki za biashara kuingiza asilimia 50
na wao wataweka asilimia 50 katika kumkopesha mkulima,” alisema na
kusisitiza kuwa serikali ya Awamu ya Tano chini Rais Dkt. John Pombe
Magufuli imeamua kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo.

Mbali ya kuipongeza serikali kwa kuzindua Mpango wa  Awamu ya Pili ya
Maendeleo ya  Sekta ya kilimo nchini (ASDP-11), Benki ya Kilimo  na
itahakikisha inafanikisha malengo ya serikali kwa ustawi wa taifa.

“Benki ya kilimo itahakikisha inawakopesha wakulima kwa riba nafuu na
kusisitiza kuwa kilimo kinalipa na hivyo Watanzania wajikite kwenye
kilimo kwa TADB ipo nyumba yao,” alisema Bw. Justine.

Naye Katibu Mkuu James alimpongeza kaimu mkurugenzi mtendaji wa benki
ya kilimo kwa hatua mbalimmbali anazozichukua  tangu alipoteuliwa na
Rais Magufuli kwa  amesimamia mambo mengi aliyoagizwa kuyafanya.

“ Benki ya Kilimo kwasasa ina fedha za kutosha kwa ajili ya kuwasaidia
wakulima nchini,” alisema Bw.James na kuongeza kuwa ni wakati mwafaka
kwa watanzania kuwekeza katika kilimo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *