TADB kuboresha zao la chikichi

TADB, MAGEREZA KUENDELEZA KILIMO CHA MICHIKICHI TANZANIA


UONGOZI wa Jeshi la Magereza umekutana na kufanya mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kwa lengo la kujadili njia na mkakati wa utekelezaji wa maagizo ya kuanzisha mradi wa kilimo na ujenzi wa viwanda vya kuzalisha mafuta ya maweze.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, baada ya kumaliza kikao hicho, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike, alisema wamekubaliana kuendeleza mradi wa kilimo cha michikichi utakaoendana na ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kuzalisha mafuta ya mawese.

Alisema katika mazungumzo ya awali, Benki ya Kilimo imeonesha nia ya kutoa mkopo wa bei nafuu utakaosaidia katika kuhakikisha kwamba mradi wa kilimo cha michikichi na ujenzi wa kiwanda vinakamilika, ikiwa ni pamoja pembejeo na vifaa vya kulimia.

“Kimsingi tumekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo kuhusu namna tutakavyotekeleza miradi ya kilimo cha michikichi pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mawese,” alisema Kasike.

Alisema Jeshi la Magereza lina maeneo mengi ya vipaumbele ambayo yakiendelezwa yanaweza kuwa na tija kwa maendeleo ya kilimo, na kuongeza kwamba anaishukuru benki hiyo, kwani iko tayari kusaidia jitihada hizo.

Mkuu huyo wa Jeshi la Magereza alisema wamekubaliana kwamba Jeshi la Magereza lifanye maandalizi ya mradi ya msingi kuhusu vipaumbele vyake kwa kuanza na mradi wa kilimo cha michikichi mkoani Kigoma.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Japhet Justine, alisema benki yake imejipanga kuwa chachu ya miradi ya kilimo yenye tija katika uchumi wa nchi na dira ya maendeleo ya viwanda.

“Tumezungumza mambo mengi, wenzetu wana maeneo mengi ambayo sisi kama benki wezeshi tuko tayari kuhakikisha kwamba wanaifikia ndoto yao ya ulishaji wa mazao ya kimkakati, ikiwamo kilimo cha michikichi kule Kigoma,” alisema Justine.

Alisema mkutano wao ni matokeo ya maagizo ya Dk. John Magufuli na Waziri Mkuu kuitaka benki hiyo kujikita zaidi katika kufadhili miradi ya kilimo yenye tija kwa taifa na kulitaka Jeshi la Magereza kuendeleza kilimo cha michikichi.

Justine alisema kwa sasa Jeshi la Magereza limebakiwa na kazi moja ya kuainisha vipaumbele na maeneo wanayotaka wasaidiwe kwa maana ya kupewa mkopo nafuu ili waweze kukamilisha mradi wao.