MKAKATI WA TADB WA KUENDELEZA MAONO YA BABA WA TAIFA MWL J. K NYERERE KWA KUFUFUA VIWANDA VYA KILIMOTarehe 11 Octoba 2019 – Ukumbi wa Kaggwa - Lindi, Tanzania

Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) yashiriki katika maadhimisho ya kumbukumbu ya baba wa taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere, yaliofanyika pamoja na maadhimisho ya kilele cha mbio za mwenge za uhuru na wiki ya vijana kitaifa na kimataifa mapema leo mkoani Lindi. Lengo kuu katika maadhamisho hayo ni kuenzi maono na urithi ambao hayati baba wa taifa Mwl. J.K Nyerere alituachia miaka 20 iliyopita. TADB imepata fursa ya kumzungumzia baba wa taifa hasa katika sekta ya kilimo, kwani aliaamini kilimo ndio maisha na hakuna maendeleo katika nchi ya Tanzania bila mapinduzi katika sekta ya kilimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB asema, Mwl J.K Nyerere alikuwa akiitazama sekta ya kilimo kwa mapana zaidi, kuanzia shambani, kiwandani hadi kwenye usafirishaji kama sekta kuu ya kuitofautisha Tanzania na nchi zingine. Kwenye miaka ya 1960, nchi ya Tanzania ilikuwa inaongoza katika kilimo cha katani na pamba, na aliamini mafanikio katika kilimo yanahitaji kuwaweka watu pamoja ndio maana alianzisha vyama vya ushirika vya wakulima, na lengo la vyama hivyo ni kumkomboa na kuwainua wakulima na misingi hiyo katika kilimo aliiweka Mwl Julius Nyerere ambayo ni endelevu na ina maslahi.

Zaidi ya 60% ya watanzania wameajiriwa katika killimo, na ili watanzania wafaidike, lazima kuwepo na kilimo chenye tija, na ndio maana Mwl JK Nyerere aliwekeza katika vyuo vya utafiti na vya kilimo ili wakulima wazidi kupata maarifa, mfano chuo cha Naliendele kilichopo mkoani Lindi, kwa ajili ya kuongeza thamani katika zao la korosho na chuo cha Luguru Mwanza kwa ajili ya zao la pamba. Na Mwl JK Nyerere, aliamini kuwa ‘juhudi bila maarifa ni juhudi za bure’ kama ilivyonukuuliwa katika kitabu cha Azimio la Arusha. Miaka ya 1980, Mwl Julius Nyerere alituonesha dira na kutupa picha ya kuendeleza sekta ya kilimo kwa kuanzisha viwanda vingi kwani bila kuwatengenezea vijana na taifa lijalo miundombinu ya kuwawezesha kiuchumi huko mbeleni, ni njia kubwa ya kubomoa uchumi na maendeleo ya taifa. Hivyo ili kuchagiza maendeleo kwa kujenga viwanda vya kuongeza thamani mahali penye malighafi, mfn. Kiwanda cha TANICA kilichianzishwa mwaka 1967. Na pia Mwl alikuwa kinyume na wakulima kuuza malighafi bali kuyapa thamani mazao ya kilimo, ndio maana katika mkoa wa Mtwara na Lindi, Mwl. alijenga viwanda vya kuchakata pamba zaidi ya 20 katika kanda ya ziwa na viwanda kubangua korosho zaidi ya 10 na kuuza nje ya nchi kama chakula au bidhaa iliyokamilika kwani ndio mkulima na watanzania watapata tija ya kilimo. Kilimo kina thamani kama kitaongezewa thamani na si kuishia shambani tu. Aliongeza ndg. Japhet Justine, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB.

Kwa kupitia maono haya, Rais JP Magufuli alianzisha taasisi mbalimbali za kilimo ikiwemo TADB ambayo itaendelea kuadhimisha maono ya hayati baba wa taifa Mwl Julius Nyerere kwa kuchagiza maendeleo ya kilimo. Na kwa sasa tumeweka mkakati wa kuanza kufufua viwanda hivi vya kuongeza thamani ya mazao na kuleta kilimo chenye tija nchini. Na tutahakikisha tunalisimamia hili ili kuinua uchumi wa nchi na wakulima waendelee kupata tija. Na ndg. Japhet Justine, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, alimalizia kwa kuwasisitiza vijana kuwa wabunifu na kutumia fursa hii ya serikali ambayo inalenga kuinua vijana wenye kuleta mapinduzi katika kujenga miundombinu.

Pamoja na hayo, benki ya maendeleo ya kilimo inaendelea kutoa huduma mbalimbali wa wakulima kwa lengo la kuchagiza maendeleo katika sekta ya kilimo nchini. Na kwa kufanikisha hilo, benki ya kilimo inawahudumia wakulima wote nchini kwa kupitia ofisi zake za kanda zilizotapakaa nchini kama Dodoma, Mwanza, Kigoma, Dar Es Salaam, na ofisi mpya za kanda ya Nyanda za Juu kusini, zitazohudumia wakulima wa Iringa na Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songwe.