TADB kutoa mikopo ya matrekta

TADB YAWATANGAZIA NEEMA WAKULIMA WANAOHITAJI MATREKTA


KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Kilimo(TADB), Bw. Japhet Justine ameshauri watanzania kujikita zaidi kwenye kilimo kwani kinalipa huku akisema benki yake ipo tayari kutoa fedha asilimia 80 kwa wanaohitaji kukopa matrekta na asilimia 20 iliyobaki itatolewa na mnunuzi.Akizungumza Kibaha mkoani Pwani mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango,Bw. Dotto James , Bw. Justine amesema benki yake imejipanga kuinua sekta sekta ya kilimo na mkulima mwenyewe hivyo matrekta yatawasidia kurahisha kazi badala ya kutumia jembe la mkono.

“Kikubwa ambacho sisi kama benki tunataka kuona mkulima anafanikiwa kupitia mazao yake na kubadilisha maisha na kujenga uchumi imara.Mkulima ana nafasi kubwa sana katika ujenzi wa uchumi wa kati na wa viwanda ifikapo mwaka 2025,” alisisitiza.Akifafanua zaidi, Bw. Justine alisema TADB imeshatoa mkopo wa Sh.bilioni 41.1 tangu kuanzishwa kwa benki hiyo na tayari ipo kwenye mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma.

“Tunatarajia kufungua tawi lingine mkoani Mbeya hivi karibuni na lengo letu ni kuwafikia wananchi popote walimo nchi nzima,” bosi wa benki alisema na kuongeza kuwa sekta ya kilimo ni muhimu sana katika sekta yeyote ya viwanda duniani. Bw. Justine alisema TADB imeingia makubaliano na Shirika la Maendeleo la Taifa(NDC) kwa lengo la kusaidia wale wanaonunua matrekta ambapo benki ya kilimo itaingiza asilimia 80 ya mkopo na mnunuzi atatoa asilimia 20.

Alisema kuwa wakulima wamefanya vizuri kwenye zao la pamba huku akielezea lengo la benki kuchoche na kuhamasisha kilimo cha kisasa zaidi ili kumuondoa mkulima kwenye jembe la mkono.“Pale tutakapofanikiwa kumtoa mkulima kwenye jembe la mkono na kumpa mashine ambazo zitamsaidia kuongeza tija, ufanisi na kumpa faida zaidi hicho ndicho benki inapenda kuona mkulima anafanikiwa,” alisisitiza.

Alisema benki yake itaanza na matrekta 500 ambayo watapewa wakulima waliofanya vema kwenye kilimo cha pamba ili kuchochea uzalishaji zaidi wa zao hilo na mazaa mengine sehemu mbalimbali nchini.“ Tuna mpango kwenda kuziambia benki za biashara kuingiza asilimia 50 na wao wataweka asilimia 50 katika kumkopesha mkulima,” alisema na kusisitiza kuwa serikali ya Awamu ya Tano chini Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeamua kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo.

Mbali ya kuipongeza serikali kwa kuzindua Mpango wa Awamu ya Pili ya Maendeleo ya Sekta ya kilimo nchini (ASDP-11), Benki ya Kilimo na itahakikisha inafanikisha malengo ya serikali kwa ustawi wa taifa.“Benki ya kilimo itahakikisha inawakopesha wakulima kwa riba nafuu na kusisitiza kuwa kilimo kinalipa na hivyo Watanzania wajikite kwenye kilimo kwa TADB ipo nyumba yao,” alisema Bw. Justine.

Naye Katibu Mkuu James alimpongeza kaimu mkurugenzi mtendaji wa benki ya kilimo kwa hatua mbalimmbali anazozichukua tangu alipoteuliwa na Rais Magufuli kwa amesimamia mambo mengi aliyoagizwa kuyafanya.“ Benki ya Kilimo kwasasa ina fedha za kutosha kwa ajili ya kuwasaidia wakulima nchini,” alisema Bw.James na kuongeza kuwa ni wakati mwafaka kwa watanzania kuwekeza katika kilimo.