Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imewasilisha taarifa ya utendaji wake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) jijini Dodoma leo tarehe 28 Agosti, 2018.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bibi Rosemary Kurwijila amesema kuwa Benki ya Kilimo imeweza kutoa mikopo inayofikia kufikia kiasi cha TZS 48.67 bilioni ikiwa ni ukuaji wa TZS 37.22 bilioni katika kipindi cha miezi saba. Ambapo hadi sasa, jumla ya wakulima 527,291 wamenufaika na mikopo ya TADB katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Tanga, Arusha, Manyara, Kagera, Zanzibar na mikoa yote inayolima pamba nchini.

Bibi Kurwijila ameongeza kuwa Ili kufikisha huduma karibu zaidi na wateja wake ikiwa ni pamoja na kuwafikia wakulima nchi nzima, TADB ilipanua wigo wa huduma zake nchi nzima mwaka 2017 na hadi sasa benki imeshafungua ofisi katika mikoa ya Dodoma ambayo ni makao makuu ya Serikali na itakayohudumia mikoa ya Kanda ya Kati na ofisi ya Mwanza itakayohudumia mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Ufunguzi wa ofisi za kanda zilizobaki umepangwa kukamilishwa katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Biashara wa Benki kati ya mwaka 2017 na 2021” alisema. Kuhusu Utoaji wa Mafunzo kwa Wakulima Wadogo Wadogo, Bibi Kurwijila alisema kuwa katika kipindi cha Julai 2017 na Julai 2018, TADB ilifanikiwa kutoa mafunzo kwa wakulima 4,434 na kufanya jumla ya wakulima waliopatiwa mafunzo tangu kuanza rasmi kwa shughuli za benki kufikia 14,450.

“Mafunzo haya yamekuwa yakilenga kuwajengea wakulima wadogo wadogo uwezo katika masuala ya usimamizi wa fedha, utunzaji wa taarifa, utawala bora wa vikundi na vyama vya wakulima, pamoja na mbinu bora za kilimo,” aliongeza. Akizungumza katika Kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine alisema kuwa Benki yake imeanzisha uratibu wa Dhamana kwa Mikopo ya Wakulima Wadogo Wadogo kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo Wadogo utakaodhamini mikopo kwa wakulima wadogo wadogo hadi asilimia 50.

“TADB imeidhinisha ushiriki wa mabenki matatu (NMB, CRDB na Benki ya Posta) ambazo zinategemewa kuanza kutoa mikopo kwa wakulima wadogo wadogo baada ya kukamilisha taratibu za kimkataba na TADB mwezi Julai 2018,” alisema. TADB ni taasisi ya maendeleo ya fedha (development finance institution) inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. TADB ni benki ya kisera iliyoanzishwa mwaka 2014 kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa fedha za mitaji midogo, ya kati na mikubwa kwenye sekta ya kilimo na kuhamasisha taasisi nyingine za fedha nchini kutoa mikopo zaidi kwa wakulima.

TADB imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni Na. 12 ya Mwaka 2002, shughuli zake zikisimamiwa na Msajili wa Hazina. Kiuendeshaji, TADB inasimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania chini ya Sheria ya Benki Kuu ya Mwaka 2006 na Sheria ya Taasisi za Fedha (Banking and Financial Institutions Act) ya mwaka 2006. TADB inatekeleza majukumu yake kama Taasisi ya Maendeleo ya Fedha (Development Finance Institution) kwa mujibu wa leseni ya biashara Na. DFI 002 iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) tarehe 4 Agosti 2015.