IMG 1812

BENKI YA KILIMO KUPELEKA MABILIONI KWENYE UMWAGILIAJI

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema itaipatia mikopo mikubwa miradi yote inayolimwa kibiashara kwa kutumia teknolojia ya umwagiliaji na kuongeza tija na kuwa na uhakika wa mazao hivyo kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchi.

Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga wakati alipotembelea na kukagua miradi ya iliyokopeshwa na Benki hiyo wilayani Kilombero mkoani Morogoro jana.

Bw. Assenga alisema kuwa ili kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka   kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini wakulima nchini hawana budi kugeukia kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza tija kilimo chao.

Bw. Assenga aliongeza kuwa matumizi madogo ya umwagiliaji katika shughuli za kilimo zimesababisha taasisi nyingi za kifedha hasa mabenki kuhofia kukopesha sekta ya kilimo nchini.

“Ili kuninua uzalishaji wenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini hakuna budi wakuliwa wageukie kilimo cha umwagiliaji ukitilia maanani nchi yetu imejaaliwa vyanzo vingi vya maji ambavyo vikitumiwa kwa busara itachagiza tija katika uzalishaji,” alisema.

Aliongeza kuwa Benki ya kilimo inalenga katika kuinua uzalishaji wenye tija katika Sekta ya Kilimo kwa kuendeleza miundombinu muhimu, mathalani: skimu za umwagiliaji, usafirishaji, hifadhi ya mazao, usindikaji, na masoko.

Kwa mujibu wa Bw. Asseanga mikopo hii italenga pamoja katika kuboresha miundombinu inayolenga kupunguza mapengo ya upatikanaji wa fedha katika minyororo ya ongezeko la thamani ya kipaumbele.

“Katika kutimiza yote haya, Benki imedhamiria kuboresha kwa upatikanaji wa mikopo na huduma za kifedha kwenye miradi ya maendeleo ya Kilimo kwa riba nafuu zilizo chini ya viwango vya kibiashara kwenye soko,” aliongeza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bw. James Ihunyo  aliwaasa wakulima hao kurudisha mikopo kwa wakati ili wakulima wengine waweze kupatiwa mikopo hiyo.

“Lengo la mikopo hiyo ni kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania, hivyo kuchelewesha mikopo hiyo kwa makusudi ni kurudisha nyuma juhudi hizi,” Bw. Ihunyo alisema.

Bw. Ihunyo aliwasihi wakulima kutambua dhamira ya serikali ya kutambua umuhimu wa kilimo kwa kuwaanzia Benki hiyo ambayo imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika  kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.

Miradi iliyotembelewa ni Kapolo AMCOS, Skimu ya Umwagiliaji ya Mkula. Nyingine ni Umoja wa Wakulima wa Miwa wa Msolwa Ujamaa na Hope ya Kidatu ambayo mpaka sasa imekopeshwa zaidi Shilingi bilioni 2 imekopeshwa kwa wakulima wa mpunga na miwa wilayani Kilombero.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *